BARUA
Barua ni mtungo unaowasilisha ujumbe kwa mtu mwengine labda kwa kutumwa kwa njia ya posta au mtu mwengine (tarishi).
Zipo aina mbili za insha za barua. Barua ya kirafiki na barua rasmi.
BARUA RASMI:
Huandikwa kwa sababu ya sababu fulani maalum. Inaweza kuandikwa kwa kuomba nafasi ya kazi, kuomba msamaha kazini, kuomba uhamisho, kuomba nafasi katika shule na kadhalika. Hushughulikia mambo rasmi na muhimu pekee.
Mtindo na muundo wake sharti ufuatilie vipengele vifuatavyo.
- Sharti iwe na anwani mbili. Moja katika upende wa kulia ya mwandishi na nyingine ya mwandikiwa. Tarehe huandikwa pamoja na anwani ya mwandishi.
- Pawe na salamu au kianzio.
- Pawe na mtajo ambao hupeana makusudio ya uandishi ambao una vianzio tofaututofauti kama vile:
- YAH: Yahusu
- KUH: Kuhusu
- KU: Kuhusu
- MINT: Mintarafu
- Katika mwili, maelezo bayana au shabaha kamili huelezewa kwa kina.
- Hitimisho, wasaalam au kimalizio huandikwa wako mwaminifu au wako mtiifu. Katika sehemu mtahiniwa atie sahihi na aandike jina lake kamili. Angalia mfano katika sehemu ya INSHA SHESHE ukurasa _______.
BARUA YA KIRAFIKI
Barua hii hususan huandikiwa ndugu awaye yule. Anaweza kuwa wa aila ya mwandishi au rafiki yeyote yule. Hutumika katika kujuliana hali au kuelezea matukio katika mandhari waliomo.
Barua hii huwa na anwani ya mwandishi upande wa kulia, tarehe vile vile chini ya anwani hiyo.
Baada ya anwani pawe na mtajo kuelekeza inaendea nani yaani mwandikiwa.
Baada ya hayo utangulizi hushughulikia salamu kwa mwandikiwa au kumjulia hali.
Aya ya pili huwa ni mtajo wa madhumuni au nia ya kuandika barua yenyewe. Vile vile mwandishi huanza kushughulikia maudhui kutoka sehemu hii kuendelea.
Hitimisho huwa ni wazo kuu kwa mwandikiwa pamoja na kumwomba mwandikiwa kuwapa wengine salamu za mwandishi.
Baada ya kukamilisha sehemu ya mwili wa insha, Mwanafunzi humalizia kwa kimalizio cha wako mpendwa, rafiki, dada, kaka, wa roho n.k. mwandishi huandika jina lake kamili.