Insha ya Methali baadhi ya uandishi unaohitaji ufundi na kusukwa kwa umakinifu. Kwanza lazima mwanafunzi aeleze maana ya nje na ndani ya methali. Ajue kuwa methali huwa na sehemu mbili; hivyo ni kusema swali na jibu au tatizo na suluhisho. Kwa mfano; Asiye na wake (swali) ana Mungu (jibu).
Atoe methali nyingine yenye maana sawa na hiyo. Baada ya hili, aandike kisa au mkasa wa kusisimua unaoambatana na Methali yenyewe. Itakuwa vizuri sana akimalizia kwa wazo kuu na methali iliyo na maana sawa na hiyo.
Tanibihi:
a) Mwanafunzi ashughulikie na ateue wahusika vizuri.
b) Anapotoa kisa au mkasa ashughulikie hadithi katika wakati wake. Asichanganye nyakati kwa mfano zipo hadithi mambo sasa na mambo zamani. Kama kisa chake kitakuwa na mwanzo wa, ‘Hapo zamani za kale…’ basi adumu katika zamani hizo asichanganye na mambo leo kama vile UKIMWI, magari, masomo n.k.
c) Iwapo hajui maana ya methali na yuajua kisa kinachoweza kulandana na wazo kuu la methali, atoe kisa moja kwa moja pasi kuandika maana ya methali. Ni vyema kufanya hivyo badala ya kutoa maana asiyoijua ipotoshe insha zaidi.
d) Aandike kisa kilicho na maadili na lugha tasfida.