Andika insha isiyopungua ukurasa mmoja u nusu kuhusu ndoto mbaya.
JINAMIZI
Nina alikuwa amenikanya kutopitia njia za vichochoroni. Siku moja, nilighairi wazo hilo na kujifanya sikio la kufa lisilosikia dawa.
Nilichapua milundi kama anayefuata mkembe aliyetoroka. Nikapitia kwenye ujia uliokuwa ukipitia katika bonde la NGAI NDEITHIA. Maana yake Rabuka ninuzuru. ‘ Lakini mama aliniambia nisiwahi pitia katika njia hii?’ Nilihisi sauti ya mahuluku wa ndani ikilonga na kunena. Hata hivyo nilipiga kifua na kujiambia kuwa waja hupitia katika ujia huu.
Ulikuwa mwendo wa saa thenashara na kila jambo lilionekana kuwa shwari bila shari. Katika safari yangu, nikakutana na mzee wa makamo. Nikamsalimia kwa heshima na taadhima kama mkembe alifundishwa akafundishika. Naye akanisalimu. Tuseme heshima si utumwa.
Nikafika chini bondeni, ambapo palikuwa na chemchemi. Palikuwa pana kichaka pande zote mbili. La ibra likatendeka. Mara kama umeme nilihisi nimeshikwa na kukamatwa. Mdomo wangu ulifungwa kwa kitambaa na nikainuliwa hobelahobela. Mimi huyoo! Nikajaribu kwa udi na ambari kujinuzuru lakini juhudi zangu ziliparamia mwamba. Nikajua waliosema kuwa mwenye nguvu mpishe hawakulenga pasipo. Kama ni wewe ungefanya nini?
Kupiga hatua chache nikaangushwa chini kama tita la kuni. Huu ulikuwa uhayawani. Lililoniogofya zaidi na kunifanya nigwaye kama kunguru ni sura matindija niliyoiona. Kutetemeka kwangu kuliongezeka nilipofikilia na kudhania ambayo yangekayofuata. Nikatabawali pasi hiari. Kijacho chembamba kikanitoka mchirizi baada ya mwingine. Nikajiuliza na kujisaili maswali sufufu. ‘ Lo! Unyama huu nitaungojea mimi siti Baraka na ni majuzi tu nimekwisha vunja ungo? Ni nani atakayeninusuru jameni? M wapi enyi waja wema? Malaika wa Mkawini m wapi? Kichaka na miti angalieni, siku ya kiama mtashuhudia.’
Niliyafumba macho yangu nisiyaona masaibu ambayo yangenisibu. Nikajihisi mfu. Mwili ukaganda kama kigaga. Nikahisi mkono ukinigusa na kupapasa. Nikashtuka nusura nisirai. Nikayatumbua macho pima kama panya aliyekwisha naswa kwa mtego. Yule baradhuli hakusema wala kunena nami. Akaendelea. Akazirarua nguo zangu. Nikadahadari kama nyoka anayekata roho. Nikaguna ndani kwa ndani kumwonyesha ananibughudhi kama mwana wa kambo. Kwa muda wa sekunde kadhaa akaendelea na udhalimu wake wa kunigusa hapa na pale. Machozi ya uchungu yakanitoka njia nne. Mara hii alikuwa karibu ….. Sauti nyororo ya nina ikanifikia. “ Siti Baraka umelala mno, amka mwanangu usije ukalimatia kufika shuleni.”
Oh! Nilikuwa nimelowa jasho. Mkojo ndio huo. Ah! Ilikuwa ndoto mbaya! Pukachaka! Itokomee mbali!