Skip to content

Kiswahili Mujarabu

Atangaye na jua hujua

  • Nyumbani
  • Yaliyomo
    • Sarufi
    • Kuandika
      • Utahini wa Insha KCPE
      • Insha Mbalimbali
      • Aina za insha
    • Kusikiliza na kuongea
    • Msamiati
    • Kusoma
  • Mawaidha ya Ufundishaji
  • Toggle search form

Rehema Za Rahimu Ni Belele

Posted on By Harun Mbijiwe 6 Comments on Rehema Za Rahimu Ni Belele

Anza kwa maneno yafuatayo: Jioni hiyo, mlango ulifunguka wazi. Sote…

REHEMA ZA RAHIMU NI BELELE
Jioni hiyo, mlango ulifunguka wazi. Sote…tulitumbua macho sawasawa na mjusikafiri aliyebanwa na mlango. Acha taharuki bin mbabaiko uzuke. Mimi, pale kochini nikatetemeka na kutetereka mithili ya nyasi nyikani wakati wa pepo za kusi. Mara bonge la mja likajitoma ndani. ‘Je tupige siahi au tuombe dua kwa Rabuka?’ Nikajisaili. Nikasali ndani kwa moyo ili Rahimu atunusuru.

Nikamtazama na kumwangalia pwagu yule. Sijawahi ona sura matindija kama ile. Alikuwa na nywele silizosokotana, uso wenye matuta ya makunyanzi, macho manene na mekundu kama ngeu, kidari na mikono iliyotutumua misuli mithili ya mchimba migodi. Alinuka fe. Kisibao alichovalia pamwe na libasi nyingine, zilikuwa chafu mno. Mikononi alishika jisu lililokuwa likimetameta. Taswira hiyo hata leo inapatikana katika kumbukumbu ya tafakuri yangu. Nikagwaya. Mimi nyumba ya udongo sihimili vishindo.

Hapo awali tulikuwa tumebishana na dada yangu kuhusu yule angeufunga mlango. Nilikaidi kabisa, naye akakataa Abadan kataan. Tulijuta majuto ya mjukuu. Methali, mkataa pema pabaya pamwita ikasadifu. Hata hivyo nikapiga bismillahi kwa Rahimu atwonee mbawazi tusije tukaangamizwa na mwizi yule.
Yule nduli alisimama kititi mbele yetu kama askari jeshi. Sauti ya radi ikatoka kinywani mwake. “Baba yenu yu wapi?”

“Ha…..yu….po, walienda pamo…ja …..” Tukamjibu huku tukitema kama kiwambo cha ngoma inapogotwa.

“Hayo yatosha!” Lile bonge la mahuluku likanikata karima.

“Basi satua ni mbili, mnyamaze mithili ya maji mtungini na mzimie zii nitekeleze wajibu wangu au mzeme jambo niwasafirishe jongomeo pasi nauli wala matwana! Mmesikia? Eh!” Yule pwagu aliashiria vitisho vyake huku akitukondolea macho yaliyokuwa mekundu kama ya mtumiaji majuni.

“Ndio.” Tulijibu sawia.

Wasaa huu, kibofu changu cha mkojo kilikuwa kimeisha salimu amri. Kochi lilikuwa limelowa mkojo. Kukuli mithaki, nilitabawali pasi hiari. Mnuna wangu alikuwa mdogo, kwa hivyo alikuwa akilia kwa shake na kite huku akinibana kana kwamba nilikuwa na msaada wake. Nikamliwaza. Tulinyamaa na kutulia pale. Simba angurumapo mcheza ni nani?

Luja yule alivuta hatua kuelekea chumbani mwa wavyere wangu. Nikafahamu na kujua, umewadia wasaa wa kujinusuru. Alipoingia upenuni tu, nikamshika dada yangu mkono. Tukafungua pujo mguu niponye. Sisi haoooo!
Kufika nje, tukapigwa na butwaa. Tukakutana na pwagu mwengine. Ikirari, asiye na bahati habahatishi. Nyoyo zetu zikawa zikawa kama za kifaranga aliyeona mwewe. Kiwewe na kimeme kikatugubika kama joho. Miguu yetu ikashindwa kustahimili uzito wa miili yetu. Nusura tuzirai. Tulikuwa tumetoka kufiwako tukaenda kuliwako nyama.

“Mnaenda wapi?” Luja yule akatuuliza.

Tukashindwa kujibu. Tukabaki tutwe mithili ya waja waliong’olewa ndimi. ‘Maskini! Afadhali tungekaa pale pale sebuleni.’ Nilijiuliza na kujisaili. Tukakaa pale huku mawazo yakitusinga na kutusonga si haba. Wahenga walikuli, mshindana na ndovu kunya hupasuka msamba.

Tukashikwa na kukamatwa. Tukaingizwa ndani na kurushwa kama magunia ya mchele. Tukatua chini ya meza. Wakwepuzi wale wakakusanya mashine za elektroniki pale sebuleni pamwe na vito vya dhamani katika vyumba kadhaa. Wakavipanga kwenye magunia na kung’oa habta. Ninashukuru mkawini faraki na ardhi kwa minajili hawakutudhulumu wala kutufanyia hiana.

Baada ya wao kung’oa nanga, nasi tukatokea chini ya meza huku tukiwa na woga wa kunguru. Hata hivyo, tulihisi vyema na kupumua. Tukakomea mlango halahala. Tukawaachia Dayani awafuate kwa maana tulikuwa tumebaki bila hata runinga. Tulikuwa tukiipenda sana kwa sababu tuliangalia na kutazama vibonzo mle.

Mwia kuduchu baadaye, tulisikia siahi. Tukasikia waja wakikimbizana kule nje. Tulishtuka, tukatetemeka na kutetereka tena kama wawele wa malaria. Nikachanganyikiwa kama ajuza katika nyumba ya densi. Nikadhani tungehirikishwa wakaa huu.

Baada ya dakika chache, tulisikia sauti ya hau akituita huku akibisha mlango. Kukamfahamu na kumtambua. Tukamfungulia. Akajitoma ndani pamwe na majirani kadhaa. Wakatua magunia yaliyokuwa yamebebwa na mapwagu dakika chache awali. Wakatupa moyo. Tukajawa na ufurufu ghaya.

Tukataka kujua ilikuwaje wakawapata waivi wale waliolazwa pale nje kama magunia. Mjomba hakusita kutuelezea vile walikuwa walikuwa wakitoka gulioni usiku huu. Walipofika langoni petu wakawafumania wezi wale. Wakapiga kabsa na ndipo majirani walipotoka kuwaauni. Wakawakamata mara moja. Kweli jirani ni akiba.

Mmoja wao alichopoa rununu na kuwaita askari. Hawakuchukua mwia mrefu kabla ya kigaro cha askari kufika na kuwasili. Wakwepuzi walibebwa hobelahobela na kupandishwa katika karandinga. Wakapelekwa katika korokoro. Vyombo kadhaa vilichukuliwa kama ithibati. Waja wakafumkana, tukabaki na mjomba kwa sababu wazazi wetu hawakuwa wamerejea kutoka safarini.Tuseme, Rahimu ni mwema. Apewe sifa kwa rehema zake. Sitahisahau siku hiyo hata nimwone nina akimkama simba buka mithili ya mbuguma.

Post Views: 186
Insha Mbalimbali

Post navigation

Previous Post: Mama Yangu Mpendwa
Next Post: Safari ya Mbuga Letaraha

Machapisho mapya

  • Barua
  • Insha ya Methali
  • Tashbihi
  • Ngeli na maelezo yake
  • Hotuba

Kumbukumbu

  • June 2025
  • January 2025
  • May 2024
  • February 2024
  • January 2024
  • September 2023
  • July 2023
  • April 2023
  • March 2023
  • September 2021
  • August 2021
  • July 2021
  • June 2021

Kategoria

  • Aina za insha
  • Insha Mbalimbali
  • Kusikiliza na kuongea
  • Kusoma
  • Majibu
  • Mawaidha ya Ufundishaji
  • Msamiati
  • Sarufi
  • Utahini wa Insha KCPE

Copyright © 2025 Kiswahili Mujarabu.

Powered by PressBook Green WordPress theme