Andika insha ya kusisimua na isiyopungua sahifa moja u nusu kuhusu safari ya kwenda katika mbuga ya wanyama.
SAFARI YA MBUGA LETARAHA
Nilipojihimu kikwara alikuwa akipiga kokoiko kuwaarifu walimwengu siku mpya imejiri. Nilichupa kutoka kwenye kitanda changu cha besera kama ngedere. Mara, mithili ya umeme nikaenda kutalii hamamu. Nikakoga yosayosa kwa maji fufutende. Nikajikwatua kwatukwatu kwa sare yangu na kujirashia marashi nikanukia hhh!
Baada ya hayo nikastaftahi chai ya mikono miwili. Nikapiga bismillahi kwa Mkawini falaki na ardhi ili aniondoshee balaa na beluwa ambazo zingenikumba safarini. Nikachukua kamera yangu, shanta ndogo na kung’oa habta. Nilichapua milundi upesiupesi nisije nikalimatia kuliwahi basi. Kukuli mithaki, chelewa chelewa utakuta mwana si wako.
Saa thenashara ushei, nilikuwa nikipiga hodi langoni pa shule. Basi lilikuwa likinguruma kuashiria matayarisho ya kung’oa nanga. Mwalimu wa Jiografia bwana Tutajua aliwasoma wanafunzi watalii hamsa wa ishirini kutoka darasa la nane waliokwisha lipa nauli ya safari hiyo. Akaongezea wengine thenashara kutoka darasa la saba. Nikajitoma pamoja nao kwenye matwana yale. Nikakaa karibu na mshikausukani. Nikatoa lawalawa nilizokuwa nimenunua siku awali na kuanza kugurugusa. Baada ya kuomba dua kwake Rabana, basi likaondoka. Walumbi waliamba, aambuaye nyayo safari ameianza.
Barasteni niliona miuja. Mbuguma wawili walikuwa wakipigana kando ya tariki. Mmoja akagongwa na kuanguka huku ameketi. Tulicheka hadi machozi yakatutoka. Kama hilo halikuwa limetosha, kupita kidogo katika mitaa ya vibanda Machomoloni, kina mama wawili walikuwa wakipigana katikati ya gurufu. Gari likasimamishwa lisije likawapiga dafrau. Kuulizia waliokuwa pale ikawa kisa na maana wakatuelezea kuwa mteja wa mwuzaji mapuya hakuwa amemlipa shilingi korija za kinywaji alichosharabu. Kukuli kuntu, ukistaajabu ya Musa utayaona ya Filauni.
Tuliendelea na safari yetu. Tukapita na kupitwa na magari aina aina. Si madogo, si makubwa, si mashangingi, si mikweche, si motokaa, si malori, si tuktuku, si pikipiki, tuseme lilikuwa jambo la kujionea si la kwambiwa.
Gari likaendelea kusonga akrabu Magharibi, baadaye likaelekea akrabu Kibla. Tukaingia nyanda za juu ambapo kuna saraa sampuri zote. Mahuluku walionekana wakilima makondeni. Wengine walikuwa waki-bak-bandika na kubak-bandua pembezoni pa barabara labda kwenda kutafuta kitumbua cha siku. Kukuli mithaki, mtu hula nguvuze.
Wakaa baada ya jua la mtikati tuliingia njia inayoelekea kwenye mbuga ya Letaraha. Ufurufu ulitujaa na kutugubika kama nina aliyepata salama. Tukapewa mwaliko na ubao uliokuwa umeandikwa, “KARIBU UVINJARI LETARAHA”. Mlinzi bwana Kuona Mengi alitukaribisha pale langoni. Wakalonga kidogo na mdarisi wetu. Tukaingia ndani kutalii. Tuseme atangaye sana na jua hujua aidha kutembea kwingi kuona mengi.
Kabla hatujasafiri parefu, mbogo akajitokeza. Ukwenzi ukapaa. Mayowe yakafuatilia ya ‘Ona!’ ‘Oneni!’ yakazindua waliokuwa wamenywea kwa safari ndefu. Mlinzi Kuona akatutahadharisha dhidi ya kupiga siahi. Nasi tukayaacha hayo. Ama kweli, mwana msikivu haonywi mara nyingi. Mbele kidogo kikundi kikubwa cha ndovu kikaonekana. Paa na ngiri hawakuachwa nyuma mithili ya koti, wakaolwa kwa mbali. Pundamilia aidha walikuwapo. Bwana Kuona kwa muda huo wote alikuwa akielezea mambo mbalimbali kuhusu hayawani hao. Nami nilukwa nikipiga picha kwa kamera yangu.
Tuliendelea kidogo. Tukala chamcha. Tukazidi na kuvinjari. Tukaona wanyama zaidi si simba aliyekuwa mawindoni, si kifaru, si twiga, si ngedere, si kulungu, hakika tulishibisha macho vya kutosha. Walioamba walikuli aliye na macho hauambiwi tazama.
Muda ulitupa kisogo. Tukaanza safari ya kurudi manzilini, huku tukiongea mengi ya yale tuliyoyaona. Siku hii ilikuwa ya kufana mno, sitahisahau hata nimwone nina akimkama simba buka mithili ya mbuguma.