Haya ni maneno yanayoficha maana ya kitu ili kisijulikane kwa urahisi. Nimeweka vichache ili kuweza kujifundisha.
A
- Adui lakini popote huendako yuko nawe – nzi
- Adui tumemzunguka lakini hatumuwezi – moto
- Afahamu kuchora lakini hajui achoracho – konokono
- Afuma hana mshale – nungunungu
- Ajenga ingawa hana mikono – mchwa
- Ajenga ingawa hana mikono – ndege
- Ajifungua na kujifunika – mwavuli
- Ajihami bila silaha – kinyonga
- Akibeba watoto wake hawezi kuwashusha – mahindi.
- Akijikunja anakuwa herufi O akijinyoosha anakua namba moja – jongoo
- Akimchukua hamrudishi – kaburi (kifo).
- Akitokea watu wote humwona – jua
- Akitokea watu wote hunungunika na kuwa na huzuni – ugonjwa
- Akivaa nguo hapendezi, akiwa uchi apendeza – mgomba
- Alipita mtu ana bunda la mshale – mkindu
- Alipita mtu mwenye kibandiko cha nguo – inzi
- Aliwa, yuala; ala, aliwa – papa
- Amchukuapo hamrudishi – kaburi
- Amefika kabla mjumbe hajarudi – nazi
- Amefunika kote kwa blanketi lake jeusi – giza
- Amefunua jicho jekundu – jua
- Ameingia shimoni akiwa uchi, akatoka amevaa nguo nzuri – mbegu
- Amejiingiza jela mwenyewe – kuku akiatamia.
- Amejitwika mzigo mkubwa kuliko yeye mwenyewe – konokono / Koa
- Amekaa kimya na watoto wamemzunguka pande zote – mgomba
- Amekula ncha mbili – wali
- Amevaa joho kubwa kuliko yeye mwenyewe – kaburi
- Ana mdomo lakini anang’ata kwa mkia – nge
- Ana miguu ya msumeno – panzi
- Anajua kuchora ingawa hajui anacho kichora – konokono
- Anakuangalia tu wala halali au kutembea – picha
- Anakula kila siku lakini hashibi na hatashiba – mchanga
- Anakula lakini hajashiba na hatashiba milele – ardhi
- Anakula lakini hashibi – mauti
- Anapendwa sana ingawaje ni mkali sana – moto
- Anatengeneza mchuzi mtamu lakini hapiki jikoni – kivuli
- Anatoka kutembea, anakuja nyumbani anamwambia mama, ‘Nieleke’ – kitanda
- Ashona mikeka wala hailali – maboga
- Askari wangu ni mpole lakini adui wanamhara – paka
- Askari wangu wote wamevaa kofia upande – majani
- Askari wangu wote wamevaa mavazi meusi – chunguchungu
- Asubuhi atembea kwa miguu mine, adhuhuri kwa miwili – fedha
- Atapanya mbegu nyingi sana lakini hazioti – mvua
- Atolewapo nje hufa – samaki
B
Babu amelala ndani ndevu zake zipo nje – mahindi
Babu amevaa koti la chuma – kobe
Bibi hatui mzigo wake – kobe / konokono
Bomu la machozi baridi – moshi
Bwana afya wa pori – fisi
C
Cheupe kimevunjika imetokea manjano – yai
F
Fuu funika, fuu funua – kutembea
G
Gari langu halitumii mafuta – miguu
H
Hana staha wala adabu kwa watu – utelezi
Hapotei hata akiwa gizani – tonge mdomoni
Hausimiki hausimami – mkufu
Hesabu yake haina faida – nywele / mchanga
Huku na huku tamu, katikati chungu – jua
Huku ng’o na huko ng’o – giza
Huuawa kwa uzazi wake – kinyonga
J
Jinamizi laniita lakini silioni – mwangwi
Juu mboga, katikati kuni, chini ugali – mhogo
K
Kaa hapa na mimi nikae pale tumfinye mchawi – kula ugali
Kafa huku akining’inia – buibui
Kamba yangu ndefu lakini haiwezi kufunga mzigo wa kuni – barabara / njia
Kila mtu atapita mlango huu – kifo
Kila mtu humwabudu apitapo – mlango
Kila niendapo hunifuata – kivuli
Kila ukiwakuta wamejitayarisha kupigana – katani / mkonge
Kilemba chake hazimishi – jogoo
Kiota chanke kimezungushiwa boma la nyasi – macho
Kipara cha babu kinafuka moshi – ugali
Kondoo wetu ana nyama nje na ngozi ndani – firigisi
Kuku wangu hutagia miibani – nanasi
Kulia kwake ni kicheko kwetu – mvua
M
Mama hachoki kunibeba – kitanda
Maskini huyu hata amechangiwa vipi haridhiki – tumbo.
Mazishi yake ni furaha kwa watu – mbegu
T
- Taa ya bure – Jua au mwezi
- Taa ya Mwarabu inapepea – Kilemba
- Tajiri aniweka mfukoni na maskini anitupa. Makamasi
- Tandika kitanga tule kunazi. Nyota
- Tangu kuzaliwa kwake sijamwona asimame wala kukimbia – Mkufu
- Tatarata mpaka ng’ambo ya mto – Utando wa baibui
- Tatu tatu mpaka pwani – Mafiga
- Tega nikutegue – Mwiba
- Teke teke huzaa gumugumu, na gumugumu huzaa teke teke – Mahindi ama yai
- Tajiri wa rangi – kinyonga
- Teketeke huzaa gumu gumu, gumu gumu huzaa teke teke – mahindi
- Tengeneza kiwanja kikubwa kabila Fulani lije kupigania – Mbono
- Tonge la ugali lanifikisha pwani – Jicho
- Tukate kwa visu ambacho hakitakatika – Maji
- Tulikaribishwa mahali na mdogo wangu, yeye akaanza kushiba kabla yangu – Kucha
- Tuliua ng’ombe na babu, kila ajaye hukata – Kinoo
- Tuliua ng’ombe wawili ngozi ni sawasawa – Mbingu na nchi
- Tumvike mwanamke huyu nguo – Kuezeka nyumba
- Tunajengajenga matiti juu – Mapapai
- Tunakwenda wote tunarudi wote lakini hatuongei – kivuli.
- Twamsikia lakini hatumwoni – Sauti
U
- Ubwabwa wa mwana mtamu – usingizi
- Ukimcheka atakucheka, ukimwomba atakuomba – mwangwi
- Ukimwita kwa nguvu hasikii, lakini ukimwita polepole husikia – fisi
- Ukimwona anakuona – jua
- Ukitaka kufahamu ana mbio, mwonyeshe moto – kinyonga
- Ukitembea ulimwengu wote utakosa nyayo – mwamba
- Ukiukata haukatiki, ukiushika haushikiki – moshi
- Ukiwa mbali waweza kumwona Fulani umatini – tundu la sindano
- Ukoo wa liwali hauna haya – wanyama
- Ule usile mamoja – kifo
- Umempiga sungura akatoa unga – funda la mbuyu
- Unatembea naye wote umjiao atakuona – bakora
- Upande wote umjiao atakuona – kinyonga
- Ushuru wa njia – Kujikwaa
- Utahesabu mchana na usiku na hutamaliza kuhesabu – nywele
- Ukisogea naye husogea, ukisimama naye husimama – kivuli
- Ukoo wetu hauishiwi na safari – siafu
- Ukumbuu wa babu ni mrefu – barabara / njia
- Utupacho wewe kwake ni dhahabu – nzi
- Viti vyote nimevikalia isipokuwa hicho – moto
W
- Wake wa mjomba kimo kimoja – vipande vya kweme
- Wakikua mama yao huwatupa mbali kwa kishindo – mbarika / nyonyo
- Wako karibu lakini hawasalimiani – nyumba ama kuta zinazoelekeana
- Waliobeba maiti hawaongei lakini yeye anaongea – chungu kinapochemka
- Wana wa mfalme ni wepesi sana kujificha – macho
- Wanakuja mmoja mmoja na kujiunga kuwa kitu kimoja – matone ya mvua
- Wanameza watu jua linapokuchwa – nyumba
- Wanamwua nyoka – watu wanaotwanga
- Wanangu wawili hugombana mchana, usiku hupatana – mlango
- Wanao wakati wao wa kuringa, nao ni weupe kama barafu – nyota
- Wanapanda mlima kwa makoti mazuri meusi na meupe – vipepeo
- Wanastarehe darini – panya
- Wanatembea lakini hawatembelewi – macho
- Watoto wa binadamu wakiondoka hawarudi – majani
- Watoto wa mtu mmoja hulala chini kila mwaka – maboga
- Watoto wa tajiri wa nguo hulala na kutembea uchi – maboga
- Watoto wangu wana vilemba, asio kilemba si mwanangu – fuu
- Watoto wangu wote nimewavika kofia nyekundu – jogoo
- Watoto wangu wote wamebeba vifurushi – vitovu
- Watu waliokaa na kuvaa kofia nyekundu – kuku, katani au mahindi
- Watu wamehama askari wekundu wakazidi nyikani – viroboto
- Watu wote ketini tumfinye mchawi – kula ugali
- Wewe kipofu unaenda wapi huko juu? – kweme
Y
- Yaenda mbali lakini haiondoki ilipo – njia
Z
- Zilitazamana na mpaka sasa hazijakutana – kingo za mto
- Ziwa dogo linarusha mchanga – chungu jikoni
- Ziwa kubwa, lakini naogelea ukingoni tu – moto
- Zulia la Mungu – ardhi.